Mazungumzo yenye lengo la kumaliza vita nchini Syria yameanza leo hii mjini Moscow, Urusi lakini kutokuwepo kwa makundi muhimu ya upinzani inamaanisha kutakuwa na matumani finyu ya kutatua mgogoro wa taifa hilo. Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Bashar al-Jaafari anaongoza ujumbe wa serikali katika mkutano huo wenye wajumbe kutoka vyama vya siasa vya ndani nchini Syria na Muungano wa Kamati ya Mabadiliko ya Kidemokrasia (NCCDC). Lakini kundi kubwa la muungano wa upinzani lenye kuungwa mkono na mataifa ya Magharibi la nje ya Syria limejiweka kando, na kundi jengine lenye kuongoza harakati za upinzani bado limo katika marufuku ya kusafiri nje ya Syria iliyowekwa na serikali ya taifa hilo. Mazungumzo haya ambayo yataendelea mpaka April 9, yanatarajiwa kujikita zaidi katika masuala ya kiutu na mipango ya mazungumzo ya siku za usoni, ambayo vilevile yanaonekana kama yanafungua njia kwa Urusi, taifa lenye kuunga mkono serikali ya Syria, kujenga taswira yake kama mpatanishi muhimu wa mgogoro wa Syria.